Kuhusu Kitengo
Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi ni miongoni mwa vitengo vya kimkakati vya Wizara ya Katiba na Sheria chenye jukumu la kuratibu na kufuatilia usimamizi wa kisheria wa utajiri asili na maliasilia za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kitengo hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sera za Taifa, sheria na maslahi mapana ya nchi, hususan Sheria ya Mamlaka ya Kudumu ya Wananchi juu ya Utajiri Asili na Maliasilia, Sura ya 449, na Sheria ya Mapitio na Majadiliano ya Masharti Yasiyo na Tija katika Mikataba ya Utajiri Asili na Maliasilia ya Nchi, Sura ya 450.
Kupitia utekelezaji wa Sheria ya Sura ya 449, Kitengo kinatekeleza dhamira ya Serikali ya kulinda na kuendeleza mamlaka ya kudumu ya wananchi juu ya utajiri asili na maliasilia za nchi. Katika kutekeleza jukumu hilo, kinasimamia utekelezaji wa misingi ya kisheria inayolinda rasilimali za Taifa dhidi ya matumizi au uhamishaji usiozingatia maslahi ya nchi, huku kikihimiza uongezaji thamani wa rasilimali ndani ya nchi, matumizi endelevu ya rasilimali na kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na maendeleo ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na utajiri huo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Sura ya 450, Kitengo huratibu, hufuatilia na kufanya uchambuzi wa kisheria wa mikataba inayohusu utajiri asili na maliasilia kwa lengo la kubaini na kushughulikia masharti yasiyo na tija kwa Taifa. Aidha, huratibu mapitio na majadiliano ya mikataba hiyo ili kuhakikisha inalinda mamlaka ya nchi, inazingatia wajibu wa Bunge katika kufanya mapitio ya mikataba, na kuweka uwiano kati ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) na kulinda maslahi ya muda mrefu ya Taifa.
Kadhalika, Kitengo huratibu na kufuatilia utekelezaji wa sera, sheria, mikakati na miongozo inayohusu usimamizi wa rasilimali mbalimbali za asili, zikiwemo madini, mafuta na gesi asilia, misitu, wanyamapori, uvuvi, ardhi, rasilimali za maji, bahari pamoja na rasilimali nyingine za kibiolojia na mazingira. Vilevile, hufanya uchambuzi wa masuala ya kisheria na kisera, huimarisha uratibu na ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na wadau mbalimbali, na kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali ili kuhakikisha utajiri asili na maliasilia unasimamiwa kwa uwazi, uwajibikaji na kwa misingi ya maendeleo endelevu.
Kupitia utekelezaji wa majukumu hayo, Kitengo huchangia kuimarisha utawala bora katika sekta ya utajiri asili na maliasilia, kulinda maslahi ya kimkakati ya Taifa, kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali na upotevu wa mapato ya Serikali, pamoja na kuhakikisha kuwa utajiri asili na maliasilia unatumika kwa manufaa ya wananchi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mawasiliano
Wizara ya Katiba na Sheria, S.L.P 315, 40484 Dodoma
📞 +255 26 2310056
🌐 www.sheria.go.tz